Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuchukue hatua Mediteranea irejee katika hali yake ya awali- Guterres

kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichokutana leo kujadili changamoto za amani na usalama kwenye ukanda wa Mediteranea. Picha: UM

Tuchukue hatua Mediteranea irejee katika hali yake ya awali- Guterres

Fursa za kiuchumi na kijamii kwenye ukanda wa Mediteranea ambao kihistoria unatambulika kwa maendeleo ya kitamaduni, hivi sasa ziko mashakani kutokana na ukanda huo kughubikwa na matatizo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema hayo akihutubia kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichokutana leo kujadili changamoto za amani na usalama kwenye ukanda huo unaojumuisha nchi zote zinazozingira bahari ya Mediteranea.

Ametaja changamoto hizo kuwa ni biashara ya madawa ya kulevya, biashara haramu ya petroli na maliasili, uharibifu wa mazingira, uhamiaji na ukimbizi pamoja na  ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto wa kike na wanawake.

Na zaidi ya changamoto hizo..

(Sauti ya Guterres)

“Mara nyingi, harakati za kukabili changamoto za usalama kwenye ukanda wa mediteranea zinatekelezwa kupitia mifumo ya kizamani ya usalama au hatua zilizozoeleka za mfumo uliopo. Aina hiyo ya hatua zina hatari ya kuendeleza hali isiyokubalika au kufanya hali iwe mbaya zaidi iwapo haziendi sambamba na juhudi za kutatua mizizi ya tatizo.”

Hivyo amesema.....

(Sauti ya Guterres)

“Tunapaswa kuazimia kabisa kutatua hali hii mbaya kwenye ukanda huu ili uweze kuendelea kuchangia vyema zaidi. Nina mategemeo yangu kwa nchi za ukanda wa Mediteranea na kwingineko kujivunia utamaduni wao wa uwazi na mshikamano.”

image
Angelino Alfano, Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia ambaye aliongoza kikao hicho kwa kuwa Italia ni rais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa mwezi Novemba 2017. Picha: UM
Italia ambayo inashikilia kiti cha urais wa Baraza hilo kwa mwezi huu wa Novemba, iliwakilishwa na Waziri wake wa Mambo ya nje Angelino Alfano ambaye amesema nchi yao iko katikati ya ukanda wa Mediteranea na imeshuhudia changamoto nyingi za usalama lakini..

(Sauti ya Angelino)

“Mkakati wetu umekuwa ni kujumuisha mshikamano na usalama. Mathalani katika janga la uhamiaji, tumedhihirisha kuwa unaweza kuokoa zaidi ya maisha nusu milioni baharini na wakati huo huo kudhibiti watu wenye misimamo mikali ambao wanaharibu maadili ya jamii  yetu ya kidemokrasia ya uwazi.”