Watoto wapewe kipaumbele katika mjadala wa uhamiaji wa kimataifa

17 Novemba 2017

Wataalam huru wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wamesema watoto wote wanaokumbwa katika zahma ya uhamiji wanapaswa kutambuliwa kwanza wao ni watoto bila kujali hadhi yao ya uhamiaji au ya wazazi wao.

Wataalamu hao wamesema hayo katika chapisho lililotolewa leo kwa minajili ya uhamiaji wa kimataifa.

Wamesema watoto ambao wanatambuliwa kuwa ni mtu yeyote mwenye umri wa chini ya miaka 18 wanaendelea kuhaha na haki zao zikikandamizwa.

Wametoa wito kwa serikali kupitisha sera na sheria mpya au zifanyie marekebisho sheria za sasa ili kutekeleza haki za watoto wote kama ilivyo katika mkataba juu ya haki za mtoto.

Bwana Benyam Dawit Mezmur ambaye ni mwenyekiti wa zamani wa Kamati ya haki za mtoto, alisema utekelezaji wa mongozo mpya sio tu jambo la haki,  ila laweza kusaidia kifichua biashara na unyanyasaji mikononi mwa wahalifu, au kunyimwa watoto wa uhuru wao kwasababu ya hali yao ya uhamiaji.