UNHCR yahofia ongezeko la mauaji ya viongozi wa kijamii Colombia

17 Novemba 2017

Shirika la Umoja wa mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limesema linatiwa wasiwasi mkubwa kutokana na ongezeko la mauaji na vitisho dhidi ya watetezi wa haki za binadamu na viongozi wa kijamii katika jimbo la pwani ya Pacific nchini Colombia ambapo wahanga katika visa vingi ni kutoka jamii za watu wa asili au za Wacolombia wenye asili ya Afrika.

Tangu Oktoba 17 alipouawa José Jair Cortés, kiongozi kutoka jamii ya watu wenye asili ya Afrika huko Tumaco, ofisi ya haki za binadamu nchini Colombia inasema viongozi saba wameshauawa na watu wasiojulikana na wengine wengi kupokea vitisho. William Spindler ni msemaji wa UNHCR Geneva.

(SPINDLER CUT)

“Kwa jumla kuna vifo 78 vinavyojulikana vya viongozi wa mashirika ya kijamii mwaka huu na vifo vingine 13 vinashukiwa, kwa njia yoyote ile hali hii inatia mashaka. Kwa kisa cha bwana Cortés’ alikuwa tayari katika ulinzi wa malaka wakati alipouawa kwa sababu ya vitisho vingi dhidi yake.”

Ameongeza kuwa jumla ya watu 15000 wametawanywa na wengine wengi wamekuwa wakiishi mafichoni hali ambayo inawafanya wakose fursa ya kuhudhuria mashamba yao au kuvua samaki ili kukidhi mahitaji yao ya msingi na kati ya Novemba 7 na 12 familia 46 zililazimika kutawanywa kwenye manisapaa za Barbacoas na Tumaco.