Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nishati ya jua yaleta ahueni kwa warohingya Cox’s Bazar- IOM

Wakimbizi waRohingya nchini Bangladesh. Picha: IOM

Nishati ya jua yaleta ahueni kwa warohingya Cox’s Bazar- IOM

Nishati ya jua imeleta nafuu katika utoaji wa huduma za afya kwenye wilaya ya Cox’s Bazar nchini Bangladesh ambako mamia ya maelfu ya wakimbizi warohingya kutoka Myanmar wamesaka hifadhi.

Shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM limesema wamechukua hatua hiyo ili kuweza kutoa huduma mchana na usiku kutokana na ongezeko kubwa la watu wanaohitaji huduma za afya.

Tangu mwezi Agosti mwaka huu zaidi ya warohingya waliosaka hifadhi eneo hilo ni zaidi ya laki 8 ambapo wanakabiliwa na matatizo ya kiafya.

Joel Millman ni msemaji wa IOM, Geneva Uswisi.

(Sauti ya Millman)

“Kabla ya nishati ya jua, huduma za afya zilitolewa mchana pekee. Hivi sasa tumeweka mpango wa kutoa huduma kwa saa 24. Nishati hii pia inasaidia kuendesha visima vya maji na mifumo ya kutakasisha maji ili kuhakikisha kuna maji safi na salama katika vituo vya afya. Halikadhalika wagonjwa wanaweza kuongeza nishati kwenye simu zao wakati wanasubiri huduma.”

Chanzo cha nishati ya jua kiliwezekana kufuatia usaidizi kampuni ya Solevolt na shirika lisilo la kifaida la Kopernik ambayo yanahusika na kusambaza nishati za gharama nafuu kwa njia zinazoendelea pamoja na kampuni ya kijamii Bangladesh, BPO.