Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres awasiliana na AU kuhusu sakata nchini Zimbabwe

Bendera ya Zimbabwe. (Picha:UN/Maktaba)

Guterres awasiliana na AU kuhusu sakata nchini Zimbabwe

Kufuatia sintofahamu inayoendelea hivi sasa nchini Zimbabwe, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema anafuatilia kwa karibu kinachoendelea huku akisihi utulivu.

Vyombo vya habari vinaripoti kuwa hivi sasa jeshi nchini Zimbabwe limeshika hatamu huku Rais Robert Mugabe akiwa ameshikiliwa ndani ya nyumba yake.

Kupitia msemaji wake Stephane Dujarric ambaye amezungumza na waandishi wa habari leo jijini New York, amesema wana wasiwasi mkubwa na kile kinachoendelea na hivyo Katibu Mkuu ..

(sauti ya Dujarric)

“Amesisitiza umuhimu wa kusaka suluhu za tofauti za kisiasa kwa njia ya mazungumzo na kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo.”

Na zaidi ya yote Bwana Dujarric amesema Katibu Mkuu..

(Sauti ya Dujarric)

“Anakaribisha hatua za jumuiya ya maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrik,a SADC za kusaka suluhu ya mzozo huo kwa njia ya amani na anaendelea kuwasiliana na mwenyekiti wa kamisheni ya Muungano wa Afrika, AU pamoja na viongozi wa kanda hiyo katika kuunga mkono jitihada hizo.”

Na kwa mantiki hiyo amesema Umoja wa Mataifa unaendelea kuunga mkono Zimbabwe katika kuimarisha utawala wa kidemokrasia.