Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP,UNICEF,WHO watoa ombi kuondoa vizuizi vya misaada ya kibinadamu Yemen

Waathirika wa mizozo yemen. Picha: UNHCR

WFP,UNICEF,WHO watoa ombi kuondoa vizuizi vya misaada ya kibinadamu Yemen

Wakuu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa leo wametoa ombi lingine la pamoja la kutaka kuondolowa haraka vikwazo ili kufikisha misaada ya kibinadamu kwa mamilioni ya watu walio hatarini Yemen.

Wakuu hao wa shirika la mpango wa chakula duniani WFP, la kuhudumia watoto UNICEF na la afya duniani WHO wamesema vizuizi hivyo vya anga, baharini na nchi kavu vimeifanya hali ya Yemen ambayo tayari ilikuwa mbaya kuwa janga kubwa na baya zaidi la kibinadamu duniani.

Wameutaka muungano nchini humo kuruhusu mahitaji muhimu kama madawa, chanjo na chakula kufikishwa kwa walengwa ili kuwanusuru na maradhi na kufa kwa njaa. Wamesisitiza kuwa la sivyo maelfu kwa maelfu ya watu wasio na hatia wengi wakiwa watoto watapoteza maisha.

Zaidi ya watu milioni 20 ikiwa ni pamoja na watoto milioni 11 wanahitaji msaada wa haraka wa kibinadamu Yemen. Angalu milioni 14.8 hawana huduma za msingi za afya, milioni 17 hawajui mlo unaofuata utatoka wapi na mlipuko wa kipindupindu umeathiri watu wapatao laki tisa, huku watoto takribani laki 4 wana utapia mlo unaotishia maisha yao.