Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano wa Vancouver wakunja jamvi kwa ahadi 46 kusaidia operesheni za mani

Kutoka kushoto kuenda kulia: Chrystia Freeland, Waziri wa Mambo ya Nje wa Canada; Harjit Singh, Waziri wa Ulinzi wa Taifa wa Canada; Jean-Pierre Lacroix, Naibu Katibu Mkuu DPKO; na Atul Khare, Naibu Katibu Mkuu DFS. Picha: M. Wells / UNNews Center

Mkutano wa Vancouver wakunja jamvi kwa ahadi 46 kusaidia operesheni za mani

Ahadi mpya lukuki za vifaa na utaalamu wa kuzifanya operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa kuwa tendaji na zenye ufanisi zaidi zimetolewa kwenye mkutano wa mawaziri wa ulinzi wa operesheni za Umoja wa Mataifa mjini Vancouver Canada jumatano .

Jumla ya nchi wanachama 79 walituma ujumbe wa mawaziri na wakuu wa majeshi kwenye mkutano huo uliojumuisha washiriki 555 kujadili changamoto kubwa na za hatari zinazokabili operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa na kuwasaidia wafanyakazi walioko mashinani katika operesheni 15 za Umoja huo duniani.

Nyingi ya ahadi hizo ni kwa ajili ya kuziba mapengo na mapungufu kama vile helkopta, na wafanyakazi wa kuendesha vifaru katika operesheni hatari zaidi ya Mali, ijulikanayo kama MINUSMA.

Canada imetangaza kwamba nchi 54 zitatia saini na kujiunga na "Kanuni za Vancouver" ili kuzuia kuajiri na matumizi ya askari wa watoto katika shughuli za kulinda amani.

Pia suala la kuongeza ushiriki wa wanawake katika operesheni hizo lilipigwa jeki kwa nchi 26 kuahidi kuhusisha mtazamo wa jinsia na kuongeza ushiriki wa wanawake. Huku mtandao mpya wa kimataifa wa kijeshi kwa ajili ya jinsia ukianzishwa kwa uongozi wa Canada, Uingereza na Bangladesh. Akizungumza katika ufungaji wa mkutano huo mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa Jean-Pierre Lacroix, amesema.

(LACROIX CUT)

“Kwa hiyo leo imeonyesha dhahiri kuwa kuna ushiriki wa pamoja, ahadi ya pamoja ya kulinda amani; kutusaidia, kufanya kazi yetu iwe na ufanisi zaidi kwa lengo moja muhimu, ambalo ni kulinda raia na kusaidia kurejesha amani. "

Naye mkuu wa Umoja wa Mataifa wa msaada mashinani Atul Khare, amewaambia washiriki alikuwa na ndoto ya kuiona dunia bila ulinzi wa amani bali yenyewe tu kuwa na amani akisema "Mpaka siku hiyo itakapowadia, lazima tuendelee kukutana" pia amewashukuru wajumbe 48, na washiriki wengine, ambao wametoa ahadi mpya za kulinda amani ambazo zinaweza kusaidia zaidi kulinda raia na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa katika ulimwengu huu ulioghubikwa na vitisho.