Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jukwaa kufanyika Geneva kujadili haki za binadamu kwenye sekta ya biashara

Ajira kwa watoto ni moja ya jambo ambalo litaangaziwa kwenye mkutano huo huko Geneva, Uswisi. (Picha:ILO)

Jukwaa kufanyika Geneva kujadili haki za binadamu kwenye sekta ya biashara

Umoja wa Mataifa umeandaa mkutano ambao kwao washiriki watajadili ni kwa jinsi gani kampuni za biashara zitazingatia haki za  binadamu pindi zinapotekeleza shughuli zao.

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu kwenye Umoja wa Mataifa Zeid Ra’ad Al Hussein amesema mkutano huo utafanyika Geneva, Uswisi tarehe 27 hadi 29 mwezi huu ukileta pamoja wawakilish kutoka kampuni kubwa, wawakilishi wa serikali, mashirika ya kiraia na wahanga wa ukiukwaji wa haki za binadamu.

Kamishna Zeid amesema jukwaa hilo litakuwa ni fursa pekee ya kuleta pamoja pande hizo kusaka suluhu ya kuzingatia haki za binadamu katika mfumo mzima wa biashara kuanzia uzalishaji hadi usambazaji.

Mathalani kwenye maeneo ambayo operesheni za kibiashara zinakiuka haki kama vile utumikishaji watoto, ubaguzi wa kijinsia na kama haitoshi wahanga wa vitendo hivyo wananyimwa haki zao.