Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi wa Rohingya wanakabiliwa na unyanyasaji na ukatili wa kingono-IOM

Takriban nusu milioni wa wakimbizi wa Rohingya wanaoishi Kutupalong wanahofiwa kunyanyazwa na kuingizwa katika biashara ya usafirishwaji haramu wa wanadamu. Picha: Muse Mohammed / IOM

Wakimbizi wa Rohingya wanakabiliwa na unyanyasaji na ukatili wa kingono-IOM

Wakimbizi wa jamii ya Rohingya waliokimbia machafuko Myanmar na kusaka hifadhi Bangladesh wananyanyaswa.

Hiyo ni kwa mujibu wa Shrika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM ambalo linaendesha juhudi za kusaidia zaidi ya wakimbizi 617,000 ambao wamewasili Cox’s Bazar tangu Agosti kufuatia operesheni za kijeshi Myanmar. Joel Millman ni msemaji wa IOM

(SAUTI YA MILLMAN)

“Wakati hakuna kipato mbadala, wakimbizi wako tayari kuchukua fursa yoyote wanayopata, ikiwemo zilizojaa hatari na zinazowagusa watoto. Pindi wanapoanza kazi, wanagundua kwamba hawalipwi fedha walizoahidiwa. Wananyimwa fursa za kulala, wanalazimika kufanya saa nyingi kuliko makubaliano, hawakubaliwi kuondoka maeneo ya kazi, hawaruhusiwi kuwasiliana na jamii zao. Wanawake na wasichana mara kwa mara wanyanyaswa kimwili na kingono.”

Kwa mujibu wa IOM unyanyasaji huo unafanyika katika vitongoji vya makazi ya wakimbizi. Aidha bwana Millman  ameongeza kwamba ni vigumu kutathmini kiwango cha unyanyasaji ambao umeripotiwa miongoni mwa wakimbizi wa Rohingya kutoka Myanmar walioko Bangladesh kabla ya wimbi kubwa kuwasili.