Madhara ya mabadiliko ya tabianchi ni dhahiri tuchukue hatua- Guterres

10 Novemba 2017

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ametaja mambo matano atakayopatia kipauembele wakati wa mkutano wa 23 wa mabadiliko ya tabianchi huko Bonn, Ujerumani.

Guterres ametaja mambo hayo akizungumza na waandishi wa habari leo jijini New York, Marekani kabla ya kuanza ziara yake Asia ambayo pia itampeleka hadi Ulaya atakakakoshiriki COP23.

Amesema mambo hayo ni muhimu kwa kuzingatia kuwa takwimu za kimataifa zinaonyesha viwango vya hewa ya ukaa ulimwenguni ni vikubwa kuwahi kufikiwa katika miaka 800,000 iliyopita na kwamba  tathmini ya tabianchi nchini Marekani inaonyesha kuwa viwango vya joto ni vya juu zaidi kuwahi kufikiwa.

Hivyo amesma akiwa Bonn atapendekeza..

(Sauti ya Guterres)

“Mosi, utoaji hewa chafuzi. Fursa ya kufikia lengo la nyuzijoto mbili inaweza kuwa na mkwamo. Tunahitaji kupunguza kwa asilimia 25 zaidi utoaji wa gesi hizo ifikapo mwaka 2020. Pili ni mnepo. Madhara ya mabadiliko ya tabianchi tayari yametufikia na yatakuwa mabaya zaidi. Tuchukue hatua zaidi watu walio hatarini waweze kuhimili. Tatu ni fedha ili tufikie kiwango chetu cha dola bilioni 100 kwa mwaka kwa nchi zinazoendelea.”

Jambo la nne ametaja kuwa ni ubia akisema anatiwa moyo kuona hatua za ubia dhidi ya mabadiliko ya tabianchi zinasonga lakini ushirikiano zaidi watakiwa. Suala la mwisho amesema ni uongozi akisema ataitisha kikao cha kuchagiza ari ya kisiasa na kiuchumi katika ngazi ya juu.