Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zambia yazindua mkakati wa ujumuishaji wananchi katika sekta ya fedha

Zambia yazindua mkakati wa ujumuishaji wananchi katika sekta ya fedha

Serikali ya Zambia hii leo kwa kushirikiana na Benki ya Dunia wamezindua nyaraka tatu muhimu zenye lengo la kuendeleza na kuimarisha sekta ya kifedha nchini humo.

Uzinduzi wa nyaraka hizo, mkakati wa ujumuishwaji wa wananchi kwenye sekta ya fedha, sera ya uendelezaji wa sekta ya fedha na ripoti kuhusu uwezo wa kifedha  umefanyika mjini Lusaka, Zambia.

Akizungumzia mkakati wa ujumuishwaji wananchi kwenye sekta ya fedha, Mwakilishi mkazi wa Benki ya Dunia kwa Zambia, Paul Noumba Um amesema hatua hiyo ni kipaumbele cha shirika lake na ni muhimu katika kutokomeza umaskini na kuimarisha ustawi.

Mkakati huo unaongeza wigo wa wananchi wanaopata huduma za kifedha kupitia matawi na mawakala wa benki na mashine za kutolea fedha.

Mathalani ametolea mfano kuwa mkakati  unaongeza vituo vya huduma za fedha kutoka takribani 7 hadi 10 kwa watu wazima 10,000.

Naye Waziri wa Fedha waZambia Felix Mutatu amesma kuimarisha sekta ya fedha nchini humo kutaruhusu wananchi kuvuna matunda ya ujumuishwa wa kifedha ikiwemo kupata mikopo kwa njia nafuu na kuweka mipango ya kukabiliana na changamoto za kifedha.