Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Urusi yageuza madeni ya Msumbiji kutoa mlo mashuleni:WFP

Urusi yageuza madeni ya Msumbiji kutoa mlo mashuleni:WFP

Mpango wa kubadili madeni kati ya Shirikisho la Urusi na serikali ya Msumbiji umeweka ahadi ya dola milioni 40 za Marekani, ambazo zitatumiwa na shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani (WFP) ili kusaidia Serikali ya Msumbiji kutoa mlo mashuleni  kwa watoto 150,000 nchini humo kwa zaidi ya miaka mitano ijayo.

Mbali na kufuta madeni kwa Msumbiji, mpango huo utatoa rasilimali mpya kwa ajili ya maendeleo na kusaidia upanuzi wa mpango wa kitaifa wa mlo shuleni ambao unalenga kutoa chakula katika shule zote za msingi nchini Msumbiji.

Hatua hiyo ya kibunifu ya Urusi ya kubadili madeni kuwa ufadhili wa maendeleo itasaidia kulisha vizazi na vizazi vya wanafunzi nchini Msumbiji kwa mujibu wa mkurugenzi mkuu wa WFP Ddavid Beasley ambaye amezishukuru serikali za Uriusi na Msumbiji kukumbatia hatua hiyo mpya ya kifedha kwa ajili ya maendeleo.

Beasley ametoa wito kwa nchi zingine wadau wa ufadhili kuangalia mkakati huo mpya bunifu ambao utasaidia kufikia malengo ya maendeleo endelevu hususani lengo la kutokomeza njaa na kufuata nyayo.