IOM yazindua huduma ya VVU katika vituo vya wakimbizi Sudan Kusini

7 Novemba 2017

Maelfu ya watu sasa watapata huduma ya ushauri, kupima na tiba dhidi ya virusi vya ukimwi, VVU nchini Sudan Kusini kufuatia shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji, IOM kuzindua huduma hizo katika vituo vya kulinda raia vya Bentiu, Malakal na Wau mwezi uliopita.

Vituo hivyo vinalenga kusaidia takriban watu 171,000 na jamii zinazowahifadhi.

IOM imesema mwaka 2016 VVU na  ugonjwa wa Kifua Kikuu vilikuwa sababu kuu ya maafa katika vituo vya kulinda raia, ambako watu wengi hawana uwezo wa kufikia vituo vya afya nje ya vituo kwa sababu ya wasiwasi juu ya usalama wao au kuharibiwa kwa miundombinu.

IOM imesema kusambaa kwa huduma ni maendeleo muhimu nchini Sudan Kusini, ambako wakimbizi wa ndani hususan wanoishi katika vituo vya ulinzi ni miongoni mwa watu wanakabiliwa na hatari kubwa ya kuambukizwa VVU.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud