Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tanzania iimarishe sekta ya maji ili kuchochea maendeleo- Ripoti

Tanzania iimarishe sekta ya maji ili kuchochea maendeleo- Ripoti

Tanzania inahitaji kuboresha haraka usimamizi wa vyanzo vyake vya maji ili uhaba wa maji usiwe kikwazo cha maendeleo.

Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti mpya ya Benki ya Dunia iliyozinduliwa jijini Dar es salaam, Tanzania ikisema kuwa uhaba wa maji hivi sasa unatokana na ongezeko kubwa la mahitaji.

Mathalani ripoti imesema kiwango cha matumizi ya maji kwa kila mtu kimeshuka kutoka mita za ujazo 3,000 miaka 25 iliyopita hadi mita za ujazo mita 1,600.

Bella Bird ambaye ni mwakilishi Mkazi wa Benki ya Dunia kwa Tanzania Malawi, Somalia na Burundi amesema hali ya sasa ikiendelea kiwango hicho kitafikia mita za ujazo 1400 mwaka 2025 na kuvuka kiwango cha mita za ujazo 1700 ambacho ni kiashiria cha uhaba wa maji na tishio kwa nchi.

Ripoti inapendekeza mambo makuu manne ambayo ni kipaumbele katika uwekezaji unaohusiana na maji, kuwekeza katika kusaka na uchambuzi wa takwimu za matumizi ya maji, kuweka bayana majukumu ya mamlaka zinazohusika na usimamizi wa maji pamoja na kuhakikisha mamlaka hizo zinapatiwa rasilimali za kutosha.

Kwa sasa sekta ya kilimo inaongoza kwa matumizi makubwa ya maji nchini Tanzania ikiwa ni asilimia 89 ilhali duniani kiwango ni wastani wa asilimia 70.