Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuna ongezeko kubwa la mashambulizi dhidi ya dini Afghanistan: UNAMA

Kuna ongezeko kubwa la mashambulizi dhidi ya dini Afghanistan: UNAMA

Kuna ongezeko kubwa dhidi ya mahali pa kuabudu, viongozi wa dini na waumini nchini Afghanistan ikiwemo mashambulizi kwenye misikiti ya Waislam wa Shia na waumini wao.

Taarifa hizo zimo katika ripoti maalumu iliyotolewa leo na mapango wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan UNAMA ikiorodhesha ongezeko la mashambulizi hayo na athari zake kwa raia.

Tangu Januari Mosi mwaka 2016 ripoti inasema raia 850 wameathirika na mashambulizi hayo 273 wakipoteza maisha na 577 wakijeruhiwa katika mashambulizi 51 yanayolenga maeneo ya kuabudu, viongozi wa dini na waumini na kwamba madhila kwa raia yameongeza mara mbili ikilinganishwa na 2009 hadi 2015.

Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa na mkuu wa UNAMA nchini Afghanistan Tadamichi Yamamoto ametoa wito wa kuheshimu sheria na kukomesha vitendo vya kuwalenga waumini na viongozi wa dini .

Pia amepongeza juhudi za serikali za hivi karibuni za kulinda maeneo ya kuabudu na kuichagiza kuchukua hatua zaidi ili kuwalinda raia wote hususani walio katika hatari ya kulengwa na mashambulizi hayo.