Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uandishi wa habari uko hatarini kote ulimwenguni-UNESCO

Uandishi wa habari uko hatarini kote ulimwenguni-UNESCO

Uandishi wa habari uko katika hatari ya kuvamiwa kote ulimwenguni ukizingatia migawanyiko ya kisiasa na mabadiliko ya teknolojia ambayo inachagiza kuenezwa kwa haraka chuki na habari bandia ambazo mara nyingi huchangia udhibiti wa uhuru wa kujieleza.

Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti ya shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO iliyotolewa leo kwa jina mwelekeo wa Dunia wa uhuru wa kujiendeleza na maendeleo ya vyombo vya habari.

Ripoti hiyo imebaini kwamba waandishi wa habari wanakabiliwa na mashambulizi ya kimwili na hata maneno na hivyo kukwamisha kazi zao. Aidha ripoti imeonyesha kuongezeka kwa visa vya kudhibiti taarifa na mtandao kote ulimwenguni na  kuongezeka kwa visa vitokanavyo na sera za kitaifa na sheria dhidi ya ugaidi vikitumika kukandamiza haki ya kujieleza.

UNESCO imesema licha ya takriban nusu ya idadi ya watu duniani kuwa na huduma ya mtandao, lakini wanawake hawawakilishwi ipasavyo kwenye vyombo vya habari kwani ni mmoja tu kati ya wanne ndiye yuko katika nafasi ya kufanya maamuzi, mmoja kati ya watatu ni mwandishi wa habari na mmoja kati ya watano anafanyiwa mahojiano kuchangia hoja.

Ripoti imesema imani na vyombo vya habari imepungua katika baadhi ya maeneo huku upinzani kutoka kwa viongozi wa kisiasa ukichangia katika udhibiti binafsi na kudidimiza uaminifu.

Halikadhalika usalama wa waandishi habari si shwari kwani 530 waliuwawa kati ya mwaka 2012 hadi 2016 wengi wakiwa katika maeneo ya Amerika ya Kati, kusini na Afrika Kaskazini, na idadi kubwa ni wanaume ambao walikuwa wakifanya kazi maeneo husika na waliripoti kuhusu jamii zao.

Hatahivyo ripoti imetaja habari njema ya kuongezeka kwa idadi ya nchi ambazo zina sheria za kuwezesha kupata taarifa na ushirikiano na UNESCO kuhusu usalama wa waandishi habari.