Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkataba wa amani Sudan Kusini ndio muarobaini wa yote- Akodjenou

Mkataba wa amani Sudan Kusini ndio muarobaini wa yote- Akodjenou

Mratibu wa kanda wa masuala ya wakimbizi nchini Sudan Kusini, Arnauld Akodjenou amesema mkataba wa amani  nchini humo ndio muarobaini wa mzozo unaoendelea nchini humo wakati huu ambapo wananchi wamechoshwa na machungu waliyopitia.

Akihojiwa na radio Miraya ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS, Bwana Akodjenou amesema simulizi za wakimbizi walio ndani na nje ya nchi hiyo zinatisha kwani wakimbizi…

(Sauti ya Akodjenou)

“Wameshuhudia baba zao wakiukawa, mama na dada zao wakibakwa mbele yao. Wakimbizi wenye umri wa kati ya miaka 13 na 20 sasa wanatumia pombe na madawa ya kulevya ili kusahau yale waliyoshuhudia. Wamepoteza kabisa matumaini ya baadaye.”

Kwa mantiki hiyo amesema mkataba wa amani wa mwaka 2015 una majawabu yote na hivyo jamii ya kimataifa ishawishi pande kinzani ziendelee na mazungumzo akisema.

image
Mtoto mkimbizi kwenye jimbo la Mto Yei nchini Sudan Kusini akiezeka paa la nyumba yao ambayo ni makazi ya muda baada ya kukimbia mzozo kwenye eneo lao. (Picha:UNMISS)
(Sauti ya Akodjenou)

“Unagusia masuala yote kuanzia usimamizi wa rasilimali asili, mipango ya uchumi, ujenzi wa taasisi na utawala pia uchaguzi. Mjadala wa sasa wa kitaifa nao lazima uwe jumuishi.”

Kwa mujibu wa mratibu huyo wa kikanda wa wakimbizi Sudan Kusini idadi ya wakimbizi sasa imefikia milioni 4 tangu kuzuka kwa mapigano nchini humo mwezi disemba mwaka 2013.