Mwaka 2017 kuvunja rekodi ya kuwa na joto kali:WMO
Ripoti mpya ya shirika la utabiri wa hali ya hewa duniani WMO iliyotolewa leo inasema inawezekana mwaka 2017 ukawa miongoni mwa miaka mitatu iliyovunja rekodi ya kuwa na jioto kali katika historia ukighubikwa na majanga makubwa kama vimbunga, mafuriko, mawimbi joto na ukame.
Ripoti hiyo ya hali ya hewa 2017 inayoainisha athari zake kwa usalama wa binadamu, maisha yao na mazingira, inasema kuna dalili za muda mrefu za mabadiliko ya tabia nchi kama vile ongezeko la kiwango cha hewa ukaa, kupanda kwa kina cha maji baharini na ongezeko la kiwango cha tindikali baharini.
Kwa mujibu wa katibu mkuu wa WMO Petteri Taalas miaka mitatu iliyopita imevunja rekodi ya joto kali duniani na 2017 joto lilikuwa wastani wa nyuzi joto 1.1C juu zaidi ya ilivyokuwa kabla ya karne maendeleo ya viwanda .
Bara la Asia likiongoza kwa kufikia nyuzi joto 50C, huku Caribbea ikikubwa na vimbunga vya kupindukia, mvua za Monsoon nazo zikisababisha mafuriko makubwa Asia, moto wa msituni ukiteketeza maisha na mali Marekani , wakati Afrika Mashariki Kenya ikitangaza ukame kama janga la kitaifa 2017.
Ripoti hii imetolewa mjini Bonn Ujeruman kwenye mkutano wa maandalizi wa COP23, na Katibu Mkuu mtendaji wa mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabia nchi UNFCCC Patricia Espinosa, ambaye ndiye mweyeji wa COP 23 amesema takwimu hizi zinaainisha ongezeko la hatari kwa binadamu, uchumi na maisha kwa ujumla, na endapo dunia itashindwa kutekeleza malengo na maazimio ya makataba wa Paris wa mabadiliko ya tabia nchi basi dunia itatumbukia pabaya.