Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP yapokea dola million 5 kutoka China kusaidia wakimbizi wa Jamhuri ya Congo na CAR

WFP yapokea dola million 5 kutoka China kusaidia wakimbizi wa Jamhuri ya Congo na CAR

Shirika la mpango wa chakula duniani WFP limepokea mchango wa dola milioni 5 kutoka China ili kutoa usaidizi wa dharura wa chakula na lishe kwa wakimbizi  wa ndani  huko Jamhuri ya Congo-Brazaville na  Jamhuri ya Afrika ya kati,  CAR.

Sixi Qu ambaye ni mwakilishi wa WFP China amesema watu zaidi ya 280,000 kutoka nchi hizo mbili watafaidika na mchango huo wa China, ambao utaiwezesha WFP kutoa mchele, mafuta ya kupikia , na vyakula maalumu vya  lishe ili kuzuia utapiamlo miongoni mwa wanawake wajawazito na watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano

WFP imesema kati ya fedha hizo, dola milioni 3 zitasaidia watu 150,000 hasa wanawake na watoto huko Jamhuri ya Congo na milioni 2 iliyobaki itatengwa kwa ajili ya majimbo ya Haute-Kotto, Basse-Kotto, Mboumou na Haut-Mbomou kusini mashariki ya CAR

WFP imesema iwapo itaendelea kupokea misaada kutoka kwa wahisani  na serikali mbalimbali duniani itaendelea kutoa  misaada ya dharura hasa kwa  walioathirika zaidi  na migogoro.