Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wasaka hifadhi huko kisiwa cha Manus wazidi kuhaha

Wasaka hifadhi huko kisiwa cha Manus wazidi kuhaha

Hofu imetanda miongoni mwa wasaka hifadhi waliosalia kwenye kisiwa cha Manus huko Papua New Guinea baada ya Australia ambayo ilikuwa inaendesha kituo hicho kutangaza kukifunga na wafanyakazi wake kuondoka.

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imeelezea wasiwasi wake kuhusu hali ya kibinadamu ya watu hao wapatao 600 waliosalia kwenye kisiwa hicho ambao wana hofu kwamba wakitoka kwenye eneo hilo wanaweza kushambuliwa na wenyeji.

Msemaji wa ofisi hiyo Rupert Colville amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi kuwa tangu Australia itangaze kufunga kituo hicho tangu tarehe 31 mwezi uliopita, hakuna huduma zozote za kimsingi za kibinadamu.

Kituo hicho kilitumika kama cha mpito katika kusubiri kupata hifadhi na sasa ofisi ya haki za binadamu imetaka Australia na Papua New Guinea zizingatie wajibu wao kwa mujibu wa sheria za kimataifa za kibinadamu na mkataba wa kimataifa wa wakimbizi wa mwaka 1951.

Bwana Colville amerejelea wito wa ofisi yake kuwa vituo vingi vinavyotumiwa na Australia kuendesha mchakato wa kupata hifadhi ikiwemo kisiwa hicho cha Manus si endelevu, vinakiuka haki za binadamu na hivyo wamesihi vihamishiwe maeneo ya bara.