Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Je tumeshindwa kuleta amani? Ahoji mkuu wa UNHCR

Je tumeshindwa kuleta amani? Ahoji mkuu wa UNHCR

Kamishna Mkuu wa shirika la kuhudumia wakimbizi duniani, UNHCR Filippo Grandi leo amehutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kuhoji iwapo jamii ya kimataifa imeshindwa kuleta amani kwani mizozo na vita inafurusha watu makwao kila uchao.

Ikiwa ni hotuba ya kwanza kwa mkuu wa UNHCR tangu mwaka 2009, Grandi amesema idadi ya watu waliolazimika kukimbia makwao imevunja rekodi na inakaribia milioni 66.

Amesema kiwango hicho ni kikubwa ikilinganishwa na wakimbizi milioni 42 mwaka 2009 akitaka mizozo ya Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo barani Afrika, bila kusahau Syria na janga la sasa la warohingya wanaokimbia nchi  yao ya Myanmar kila uchao na kukimbilia Bangladesh.

(Sauti ya Grandi)

“Je tumeshindwa kufanya mashauriano na kuleta amani? Nauliza swali hili hapa mbele ya Baraza la Usalama, ambalo msingi wake wa kuwepo ni amani na usalama, kwa sababu nashuhudia madhara ya moja kwa moja ya kushindwa huku, kila siku mamilioni ya watu wanalazimika kukimbia makwao wakiwa na matumaini finyu ya kuweza kurejea makwao kwa vizazi kadhaa.”

Akaenda mbali zaidi kutoka mifano ya madhila anayoshuhudia..

image
Budoor, mkimbizi kutoka Syria mwenye umri wa miaka 15, akiwa anaangalia anga kwa lengo la kulichora. Mkimbizi huyu katika kambi ya Azraq nchini Jordan lengo lake ni kuwa mwanaanga.
(Sauti ya Grandi)

“Wanawake wanahaha peke yao kuhudumia watoto wao kwenye makazi ya muda bila kuwepo kwa faragha ya kutosha, wapenzi wao wanapoteza maisha au wamepotea. Wazee wanashuhudia maisha yao yakifikia ukingoni kwenye nchi ambazo si zao.”

Kwa mantiki hiyo Mkuu huyo wa UNHCR amependekeza mambo manne kwa Baraza la Usalama..

(Sauti ya Grandi)

“Mosi msaidie harakati za kuzuia mizozo na kuepusha majanga yatokanayo na ukimbizi. Pili ulinzi wa amani uimarishwe sambamba na kuweka fursa kwa watoa huduma za misaada na kulinda raia kwenye mizozo. Tatu, jamii ya kimataifa ichukue hatua kulinda wakimbizi kutumbukia katika mikono ya wasafirishaji  haramu wa binadamu. Wasafirishaji wakamatwe na wafikishwe mbele ya sheria. Nne ni muhimu kuendeleza ulinzi dhidi ya watu waliopoteza makazi na pia jamii za wenyeji ambao wanawahifadhi.”