Ugonjwa wa kuhara bado tishio kwa watoto Afghanistan- UNICEF

2 Novemba 2017

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF limesema ugonjwa wa kuhara umesalia tishio miongoni mwa watoto nchini Afghanistan ingawa idadi ya vifo vimepungua kwa mara ya kwanza na kuwa chini ya 10,000 wakati huu.

Saidi Adele Khodr ambaye ni mwakilishi wa UNICEF Afghanistan amesema ugonjwa huo ni tishio kwa kuwa kila siku husababisha vifo vya watoto 26.

Hata hivyo amesema vifo hivyo vinaweza kuepukwa kirahisi watu wakizingatia usafi wa mazingira ikiwemo  matumizi ya vyoo na hata kunawa mikono kila mara.

Kutokana na jitihada za UNICEF, wilaya ya Nili, katika jimbo la Daykundi, ilitangazwa tarehe mosi mwezi huu kuwa eneo ambalo hakuna mtu anayejisaidi katika eneo la wazi, ikiwa ni kampeni ya kutokomeza ugonjwa wa kuhara.

UNICEF na washirika   wake  wanatoa wito kwa wilaya zote nchini kuchukua hatua za kudhibiti  ugonjwa huo na  kuunga mkono harakati ya kuboresha na kuokoa maisha ya watoto walio katika  mazingira magumu.

Aidha  UNICEF imesema ukosefu wa  amani na usalama katika sehemu mbalimbali Afghanistan  unaendelea kuathiri upatikanaji wa huduma za kibinadamu katika baadhi ya maeneo nchini,  hivyo kupunguza kasi ya maendeleo.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter