Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Serikali zikomeshe mashambulizi dhidi ya wanahabari

Serikali zikomeshe mashambulizi dhidi ya wanahabari

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya kutokomeza ukwepaji sheria wa vitendo vya  uhalifu dhidi ya waandishi wa habari, imeelezwa kuwa maisha ya waandishi wa habari yamesalia hatarini hata wanapokuwa katika harakati za kuandika habari kwenye maeneo yao.

Katika ujumbe wake wa siku hii, Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO Irina Bokova ametolea mfano kipindi cha kuanzia mwaka 2006 hadi mwaka jana ambapo waandishi wa habari 930 waliuawa.

Amesema asilimia 93 ya waandishi hao wa habari waliuawa kwenye nchi zao wakati wanaandika habari kuhusu maeneo hayo.

Bi. Bokova amesema cha kusikitisha zaidi ni kwamba katika kila visa 10 ni kisa kimoja tu ambacho kinaripotiwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria huku waandishi wa habari wa kike wakikumbwa na manyanyaso zaidi mitandaoni.

Mkurugenzi Mkuu huyo wa  UNESCO amesema ni muhimu serikali ziimarishe utawala wa sheria na uongozi bora na kusongesha malengo ya maendeleo endelevu hususan lengo namba 16 linalopigia chepuo amani, haki na taasisi thabiti.

image
UNESCO inasema wanahabari wa kike nao wanakumbwa na majanga zaidi kwa kuwa wanakabiliwa pia na mashambulizi kupitia mitandao. (Picha:UN/Tobin Jones)
Wakati huo huo, wataalamu huru wa Umoja wa Mataifa wametaka kukoma mara moja kwa mashambulizi dhidi ya wanahabari wa vyombo mbalimbali pamoja na mabloga.

Wataalamu hao Agnes Callamard anayeangazia vitendo vya watu kukamatwa kiholela na kuuawa hovyo pamoja na David Kaye wa haki ya uhuru wa kujieleza wamesema serikali lazima zichukue hatua.

Wamesema jamii haziwezi kuendelea kuvumilia kuona ongezeko la kasi ya mashambulizi dhidi ya waandishi wa habari na hivvyo serikali ziwekeze kukomesha mwenendo huo.