Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchi 191 zaunga mkono kuondolewa Cuba iondolewe vikwazo, Marekani na Israeli wapinga

Nchi 191 zaunga mkono kuondolewa Cuba iondolewe vikwazo, Marekani na Israeli wapinga

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na mjadala wa wazi kuhusu umuhimu wa kuondoa vikwazo vya kiuchumi, kibiashara na kifedha vilivyowekwa na Marekani dhidi ya Cuba.

Kura ya leo ambayo imepigwa kwa miaka 26 mfululizo imepitishwa na nchi 191 wakiunga mkono kuondolewa kwa vikwazo hivyo huku Marekani na Israeli wakipinga azimio hilo, safari hii ikiwa ni tofauti na hali ya mwaka jana wakati nchi hizo mbili hazikuonyesha msimamo wowote katika kura ya mwaka 2016 ikiwa ni mara ya kwanza katika kipindi cha robo karne.

Akikanusha hoja ya kutengwa ambayo ilitumika na nchi yake mwaka jana, mwakilishi wa kudumu wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Nikki Haley amesema iwapo watu wa Cuba wataendelea kunyimwa haki za kibinadamu na haki za msingi na iwapo mapato ya Cuba yataendelea kuimarisha utawala wa kidikteta ambao unawanyima wananchi haki hizo, basi Marekani haiogopi kuwa pweke katika Baraza hilo au kwingineko.

Kwa upande wake waziri wa mambo ya nje wa Cuba Bruno Rodríguez Parrilla, amesisitiza kwamba serikali ya Marekani haina mamlaka ya kuihukumu nchi yake wakati yenyewe ikifanya vitendo vya unyanyasaji na ukiukaji wa haki za binadamu. Halikadhalika amekumbusha kwamba raia wa Marekani hawakubaliani na vikwazo hivyo kama ilivyo kwa nchi zingine.

Ameongeza kwamba vikwazo hivyo ni kizuizi kikubwa katika ukuaji wa kiuchumi na kijamii wa Cuba na kwamba kuanzia Aprili 2016 hadi Aprili 2017 vilisababisha hasara ya takriban dola milioni 4,300 kwenye uchumi wa Cuba.