Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO na MONUSCO wasaidia wahanga wa kipindupindu DRC

WHO na MONUSCO wasaidia wahanga wa kipindupindu DRC

Nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC, shirika la afya ulimwenguni WHO na ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, MONUSCO wamewasilisha dawa kwa wahanga wa mlipuko wa ugonjwa kipindupindu kwenye eneo la Walikale, jimbo la Kivu Kaskazini, ugonjwa ambao umesababisha vifo vya watu 29 ndani ya wiki tatu.

Usaidizi huo unaofuatia ombi kutoka serikali ya jimbo hilo ni pamoja na kilo 700 za dawa kwa ajili ya wagonjwa kwenye kitongoji cha Oninga kilichopo kilometa takribani 300 kutoka mji wa Walikale.

Kwa wiki tatu sasa wakazi wa eneo hilo wamegubikwa na Kipindupindu ambapo walinda amani wa MONUSCO wamesaidia kuimarisha ulinzi dhidi ya vikundi vilivyojihami ambavyo vimekuwa vikinyanyasa wakazi hao.

Ulinzi huo kutoka MONUSCO umesaidia dawa hizo kuwasilishwa kwenye vituo vya afya vinavyohudumia wakazi wapatao 11,000.

Mmoja wa wauguzi katika vituo hivyo Samuel Musambia ameieleza MONUSCO kuwa changamoto waliyo nayo sasa ni ukosefu wa vituo vya kuwatenga wagonjwa wa kipindupindu pamoja na watu kutozingatia usafi, mambo ambayo yanasababisha maambukizi kuenea haraka.