Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tume ya haki za binadamu CERD kujadili changamoto za ubaguzi wa rangi

Tume ya haki za binadamu CERD kujadili changamoto za ubaguzi wa rangi

 Tume ya  haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa  inayopiga vita ubaguzi wa rangi CERD imesema chimbuko la  ubaguzi wa rangi, ambalo ni matokeo ya ukoloni, pamoja matukio mbali mbali yanayotokea duniani hivi sasa toka kwenye makundi yenye msimamo wa kibaguzi, yanazidi kuchochea  ubaguzi wa rangi ulimwenguni kote.

Akizungumza katika kikao cha 72 cha bazaka kuu la  Umoja wa Mataifa, mwenyekiti wa tume hiyo Anastasia Crickley ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kushughulikia ubaguzi wa rangi, ikiwa ni pamoja na kuchukua  hatua maalumu, dhidi ya waathirika wa  ubaguzi unaoendelea, ikiwa ni pamoja na watu wa asili ya Kiafrika, jamii ya Roma, watu wa asili na watu wa dini ya  kiislamu.

Aidha bi Anastasia akitolea mfano wa Afrika kusini akisema, ubaguzi wa rangi ulipigwa vita na kushindwa, haki za kiraia zilipatikana, hivyo Umoja wa Ulaya una wajibu wa kulinda watu dhidi ya ubaguzi wa rangi katika nchi wanachama kutokana na sheria za kukabiliana na ubaguzi wa rangi katika makubaliano ya nchi 178 ambazo zimeridhia mkataba wa CERD.

Katika kikao hicho bi Anastasia amelaani vitendo vya  viongozi wa kisiasa ambao hutumia jukwa la kisiasa kuchochea chuki au kushindwa kukemea mashambulizi ya ubaguzi wa rangi katika nchi zao. Pia ametoa wito kwa  nchi 11 ambazo bado hazija saini mkataba wa kimataifa wa kupiga vita  aina zote za ubaguzi wa rangi kufanya hivyo haraka.

Tume hiyo  itatumia nusu ya siku ya tarehe 29 Novemba 2017 huko Geneva kujadili ubaguzi wa rangi na changamoto  zake katika ulimwengu wa leo.