Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Walinda amani wauawa DRC, MONUSCO yaonya ADF

Walinda amani wauawa DRC, MONUSCO yaonya ADF

Walinda amani wawili wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, MONUSCO wameuawa na wengine wamejeruhiwa kufuatia shambulio la hivi karibuni kwenye kitongoji cha Mamundioma, karibu na mji wa Beni, jimbo la Kivu Kaskazini.

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini DRC na mkuu wa MONUSCO Maman Sidikou amesema shambulio hilo lilitekelezwa na waasi wa kikundi cha ADF.

Hata hivyo amesema MONUSCO waliweza kudhibiti na kupunguza maafa kwa raia na kwa watendaji wake, na majeruhi wamepelekwa Goma kwa matibabu.

Shambulio hili la karibuni linafuatia shambulio la jumapili ambapo ADF walishambulia msafara wa raia na kuua raia 20.

Bwana Sidikou amelaani mashambulizi dhidi ya raia na walinda amani wa Umoja wa Mataifa kwenye eneo hilo la Beni akikumbusha kuwa MONUSCO itakabiliana navyo.

Tayari MONUSCO imeimarisha usalama kwenye eneo hilo ili raia waweze kuendelea na shughuli zao.