Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Juhudi zaidi zinahitajika ili kuwekeza katika kawi inayojali mazingira-UNEP

Juhudi zaidi zinahitajika ili kuwekeza katika kawi inayojali mazingira-UNEP

Serikali na asasi za kiraia zinahitaji kuongeza juhudi kuhakikisha kwamba makubaliano ya mkataba wa mabadiliko ya tabianchi wa Paris yanafikiwa.

Akizungumza hii leo wakati wa uzinduzi wa ripoti ya nane kuhusu uchafuzi wa hewa kuelekea mkutano wa mabadiliko ya tabianchi huko Bonn, Ujerumani mkurugenzi mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa mazingira, UNEP  Erik Solheim amesema ikiwa ni mwaka mmoja tangu mkataba huo kutiwa saini, bado mambo mengi yanasalia katika kuokoa mamia ya mamilioni ya watu kuepukana na mustakabali wenye madhila.

Kwa mujibu wa ripoti, kufikia sasa ahadi za mataifa zitapunguza uchafuzi wa hewa kwa theluthi moja tu ya viwango vinavyohitajika ili kufikia malengo.

Bwana Solheim ameongeza kwamba ruzuku kwa viwanda vya mkaa na gesi inapaswa kufutwa ili kuchagiza uwekezaji katika kawi inayojali mazingira ili kudhibiti joto la hewa

(Sauti ya Solheim)

“Ruzuku yoyote ya nishati ya kisukuku iwe ni mkaa, mafuta au gesi inapaswa kuwekwa. Hatuwezi kuendelea kutenga ruzuku kwa kitu ambacho hakitakiwi. Kile ambacho tunaweza kufanya ni kutoa fursa za kuanza kwa vitu tunavyohitaji ambavyo ni nishati jua, upepo maji na kioevu na nyinginezo.”

Halikadhalika amesema iwapo Marekani itajiondoa kutoka mkataba wa Paris mwaka 2020, hali itakuwa mbaya zaidi.

Ripoti imeorodhesha mbinu za kuweza kupunguza uchafuzi wa hewa kupitia hatua za kuimarisha udhibiti katika sekta mbali mbali ikiwemo, kilimo, ujenzi, kawi, misitu, viwanda na usafiri.