Skip to main content

Dawa za kuua wadudu mashambani zahatarisha maisha ya barubaru

Dawa za kuua wadudu mashambani zahatarisha maisha ya barubaru

Katika juhudi za kuchangia kulinda sayari dunia dhidi ya uchafuzi, wataalam na wasimamizi wameungana na wanachama wa mkataba wa Rotterdam na Stockholm wa kamati ya kutathmini kemikali mashambani huko Roma, Italia kutathmini baadhi ya kemikali zitakazojumuishwa katika mikataba miwili inayolenga kulinda afya ya binadamu na mazingira.

Mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa lile la chakula na kilimo duniani FAO na la mpango wa mazingira UNEP yametoa tangazo hilo leo, yakisema kwamba kemikali tatu nyingine zimependekezwa kuingizwa katika mkataba wa Rotterdam huku mbili nyinigine zikipendekezwa kwenye mkataba Stockholm.

Kwa mujibu wa takwimu, za FAO, mauzo ya kimataifa ya dawa za kuua wadudu kwenye mimea yaani viuadudu yanagharimu dola bilioni 480 kwa mwaka.

UNEP inakadiria kwamba zaidi ya asilimia tatu ya watu wanaofanya kazi katika sekta ya kilimo kote ulimwenguni wanaathirika kutokana na matumizi ya viuadudu, huku barubaru wakikabiliwa na hatari zaidi.

Mkataba wa Rotterdam ambao kwa sasa una wanachama 159 unatoa tahadhari ya mapema kuhusu mauzo ya baadhi ya kemikali na viuadudu kupitia utaratibu wa makubaliano ya awali, mfumo unao hitaji wadau kuchukua maamuzi kuhuzu uagizaji wa kemikali katika siku zijazo.