Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jukwaa laanza Bahrain likiangazia ujasiriamali na SDGs

Jukwaa laanza Bahrain likiangazia ujasiriamali na SDGs

Jukwaa la kimataifa kuhusu uwekezaji katika ujasiriamali linaanza leo huko Manama nchini Bahrain kwa lengo la kuimarisha uhusiano kati ya uwekezaji, ujasiriamali na malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

Katika ujumbe wake kwa njia ya video kwa washiriki wa jukwaa hilo lililoandaliwa na shirika la maendeleo ya viwanda la Umoja wa Mataifa, UNIDO na wadau wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema..

(Sauti ya Guterres)

“Nawapongeza kwa jukwaa la mwaka huu kuangazia malengo ya maendeleo endelevu. Maendeleo endelevu ya viwanda ambayo pia ni shirikishi yataendelea kuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo na tunaunga mkono nchi wanachama katika kazi hii adhimu.”

UNIDO imesema jukwaa hilo linafanyika Bahrain kwa kuzingatia jinsi nchi hiyo iko mstari wa mbele kusongesha ujasiriamali kama njia ya kufanikisha amani, ustawi na uwezeshaji wa kiuchumi duniani.

Na ni kwa mantiki hiyo Katibu Mkuu Guterres amerejelea ufunguzi wa kwanza wa ofisi ya uwekezaji na maendeleo ya teknolojia huko Manama mwaka 1996 akisema kuwa kwa miaka kadhaa sasa mfumo wa Bahrain umetengeneza zaidi ya fursa 16,000 za ajira na uwekezaji wenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 2.

Kwa mujibu wa Guterres hii leo nchi 52 zinaendeleza muundo wa ujasiriamali na kubadilisha vyema maisha ya wananchi.

Jukwaa hilo litamalizika tarehe pili mwezi ujao wa Novemba.