Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sahel pamoja na usalama wanahitaji maendeleo endelevu- Guterres

Sahel pamoja na usalama wanahitaji maendeleo endelevu- Guterres

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na kikao cha ngazi ya mawaziri kuhusu jinsi jamii ya kimataifa inaweza kusaidia operesheni za kikosi cha pamoja cha nchi tano za ukanda wa Sahel barani Afrika, G5.

Akihutubia kikao hicho, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema kwa kuangalia udharura wa hali ilivyo kwenye ukanda huo, kuna umuhimu wa kusaidia nchi hizo tano siyo tu kiusalama, bali pia mikakati ya kimaendeleo.

Bwana Guterres amesema muda unaenda kasi na hivyo ni lazima jamii ya kimataifa kuibuka na mbinu bunifu kusaidia eneo hilo ambalo linakabiliwa na changamoto za kiusalama, kibinadamu, kiuchumi na kisiasa.

Amesema kwa kuwa tayari nchi hizo tano ambazo ni Mali, Mauritania, Niger, Burkina Faso na Chad, zimeonyesha ni za kumaliza changamoto zinazowakabili, ni lazima kuwasaidia akisema Umoja wa Mataifa kwa upande wake..

(Sauti ya Guterres)

“Mwezi disemba wakati wa mkutano wa Brussels kuhusu Sahel, tutawasilisha mkakati wa uwekezaji kwenye ukanda wa Sahel. Natumai tunawategemea msaada wenu na wadau wetu wote. Ningependa pia kutoa wito wa ushirikiano zaidi kati ya mifumo ya kitaifa, kikanda na kimataifa. Uthabiti wa utawala wa kisheria pekee ndio unaweza kuhakikisha uendelevu wa mikakati hii. Na katika mazingira hayo magumu, ina maana kwamba kusaidia kazi za wafanyakazi wa misaada na mashirika yanayojitolea kufanikisha maendeleo endelevu.”

Kikao hicho kilihudhuriwa pia na wajumbe wa nchi hizo tano za Sahel na kimefanyika baada ya ziara ya wajumbe wa Baraza la Usalama mwishoni mwa wiki iliyopita.