Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kiwango cha hewa ukaa kimefurutu ada-WMO

Kiwango cha hewa ukaa kimefurutu ada-WMO

Viwango vya hewa ya ukaa hewani na kwenye mazingira vimeongezeka mwaka 2016 na kufikia kiwango cha juu zaidi kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 800,000 kwa mujibu wa Shirika la hali ya hewa duniani, WMO. Assumpta Massoi na taarifa kamili

(TAARIFA YA ASSUMPTA)

Shirika la WMO limesema kupitia taarifa iliyotolewa leo kwamba kote ulimwenguni viwango vya hewa ya ukaa vimeongezeka kwa sababu zitokanazo na binadamu na matokeo ya El Niño. Kufikia sasa viwango vya hewa ukaa ni asilimia 145 ikilinganishwa na kabla ya enzi za viwanda .

Ongezeko hilo ambalo linachangiwa na mambo kadhaa ikiwemo kuongezeka kwa idadi ya watu, kuimarika kwa kilimo, kuimarika kwa matumizi ya ardhi na ukataji miti, ukuaji wa viwanda na matumizi ya kawi itokanyao na mimea linauwezo wa kuleta mabadiliko ya tabianchi na kuleta matatizo makubwa ya kiikolojia na kiuchumi.

Katibu Mkuu wa WMO Petteri Taalas ameonya iwapo viwango vya hewa ukaa havitapunguzwa malengo yaliyokubaliwa kufuatia makubaliano ya mkataba wa mabadiliko ya tabianchi wa Paris kufikia mwisho wa karne hii hatatimia na athari zake zinaongezeka ikiwa ni pamoja na

(SAUTI TAALAS)

“Kuchangia zaidi ya asilimia 60 ya joto duniani, pia mabadiliko katika mfumo wa hali ya hewa, athari katika mfumo wa mvua, kuna ukame mkubwa katika baadhi ya sehemu duniani, moto wa msituni, changamoto katika kilimo na pia kuna mafuriko katika baadhi ya sehemu duniani na vyote hivyo vinachagizwa na mabadiliko ya tabia nchi.”