Usaidizi zaidi wahitajika Yemen- Lowcock

28 Oktoba 2017

Mwishoni mwa ziara yake ya siku tano huko Yemen, Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu Mark Lowcock, amesisitiza umuhimu wa usaidizi zaidi wa kifedha ili kukidhi mahitaji ya wananchi.

Halikadhalika ametoa wito kwa pande kinzani kwenye mzozo nchini Yemen kuzingatia sheria za kibinadamu za kimataifa za ulinzi wa raia kwenye mizozo pamoja na wafanyakazi wa misaada.

Bwana Lowcock akizungumza mjini Sana’a amesema ameshuhudia hali ya kutisha ya kibinadamu huko Aden, Sana’a, na katika majimbo ya Lahj, Hudadydah, Hajjah, na  Amran ambako mamia ya wayemen wana simulizi za machungu.

Mkuu huyo wa OCHA amesema amekuwa na mazungumzo ya dhati na ya kina na serikali mjini Aden na pande kinzani huko Sana’a kuhusu mbinu za kupunguza machungu ya wananchi.

Mathalani amesema mjini Aden amemsihi Waziri Mkuu kuhakikisha pamoja na mambo mengine wanalipa mishahara ya wahudumu wa afya, elimu na watumishi wengine wa serikali bila kusahau kufungua uwanja wa ndege wa Sana’a kwa ajili ya ndege za biashara na za huduma za kibinadamu.

Kwa upande wa wapinzani huko Sana’a ameeleza hofu yake juu ya mazingira magumu ya utendaji kwa Umoja wa Mataifa na mashirika ya misaada akisema kila mara harakati zao zinakumbwa na vikwazo.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud