Mkuu wa WFP yuko ziarani DRC kutathimini hali ya chakula

27 Oktoba 2017

Mkurugenzi mkuu wa shirika la Umoja wa mataifa la mpango wa chakula duniani (WFP) bwana David Beasley, leo amewasili nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC kwa ajili ya ziara ya siku nne wakati hali ya kibinadamu kiendelea kuzorota nchini humo.

Bwana Beasley atatathimini athari za vita kwa uhakika wa chakula na lishe na juhudi za WFP na mshirika mengine katika kupambana na janga la njaa linaloibuka.

Kesho Jumamosi atakutana na familia zilizoathirika na kutawanywa kutokana na machafuko huko Kusini-Kati mwa jimbo la Kasai ambako zaidi ya watu milioni tatu sawa na robo ya watu wote wanakabiliwa na tatizo la uhakika wa chakula tangu kuzuka kwa ghasia katikati ya mwaka 2016.

Jumapili atakuwa jimboni Kivu Kaskazini kutathimini ugawaji wa chakula wa muda mrefu kwa watu waliotawanywa na vita na pia atazuru kituo kinachotoa msaada wa lishe kwa wanawake na watoto.

Na siku ya mwisho Jumatatu atakaporejea Kinshasa , Beasley atabadilishana mawazo na wajumbe wa serikali, maafisa wa Umoja wa Mataifa na wawakilishi wa jumuiya ya wahisani, na pia waandishi wa habari watapata fursa ya kuzungumza naye.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter