Surua yaendelea kudhibitiwa lakini bado ni tishio- WHO

27 Oktoba 2017

Idadi ya vifo vitokanavyo na ugonjwa wa surua ilipungua kwa asilimia 84 mwaka jana ikilinganishwa na mwaka 2000, sababu kuu ikiwa ni chanjo dhidi ya ugonjwa huo.

Ripoti ya mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo lile la afya, WHO, la watoto UNICEF na ubia wa chanjo duniani, GAVI imesema mwaka jana waliofariki dunia kwa surua ni watu 90,000 ikilinganishwa na watu zaidi ya 550,000 miaka 10 iliyopita.

Mashirika hayo yamesema hii ni mara ya kwanza kwa idadi ya vifo vitokanavyo na surua kuwa chini ya 100,000 kwa mwaka.

Dkt. Robert Linkins ambaye ni mtaalamu dhidi ya surua na rubella kutoka mpango wa pamoja wa Marekani, na mashirika ya Umoja wa Mataifa, MR&I amesema kuokoa wastani wa vifo milioni 1.3 kwa mwaka kutokana na chanjo dhidi ya surua ni mafanikio makubwa.

Tangu mwaka 2000, takribani chanjo bilioni 5.5 zimepatiwa watoto kupitia mfumo wa kawaida wa utoaji chanjo kwa watoto na kampeni na hivyo watu milioni 20.4 wameokolewa.

Kwa upande wake Dkt. Jean-Marie Okwo-Bele, mkurugenzi wa chanjo WHO amesema sasa mwelekeo ni kutokomeza kabisa ugonjwa huo na hilo linawezekana kwa kuhakikisha kila mtoto anapata chanjo.

Hadi sasa watoto zaidi ya milioni 20.8 wanakosa dozi yao ya kwanza ya chanjo dhidi ya surua na zaidi ya nusu yao wako katika nchi sita.

Nchi hizo ni Nigeria, India, Pakistan, Indonesia, Ethiopia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter