Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Marekani yataka Sudan Kusini ichukue hatua kulinda raia

Marekani yataka Sudan Kusini ichukue hatua kulinda raia

Mwakilishi wa kudumu wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Nikki Haley amekuwa na ziara ya ghafla nchini Sudan Kusini ili kutathmini matumizi ya misaada ya fedha inayotolewa na nchi yake kwa nchi hiyo ya Afrika.

Akiwa nchini humo ametembelea kambi ya kuhifadhi raia yenye jumla ya wakimbizi wa ndani zaidi ya 33,000 ambapo amesema alichoshuhudia si alichotarajia.

Amesema walidhania kuwa wanawekeza kwenye nchi ambamo kwayo watu watakuwa huru na salama lakini hali haikuwa hivyo.

Balozi Haley ameseam Marekani imewekeza zaidi  ya dola bilioni 11 Sudan Kusini lakini amevunjika moyo kutona hali ngumu ya wananchi hasa kwenye kituo hicho kilichopo mji mkuu Juba.

Amesema amekuwa na mazungumzo na Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini na ameahidi kuleta mabadiliko.

Balozi Haley amesema amewajulisha kuwa sasa ni wakati wa kuchukua hatua ili kuona mabadiliko na kwamba Rais Kiir achukue hatua kwa maslahi ya wananchi wake.

Wakati wa ziara hiyo, wakimbizi wa ndani kwenye kituo hicho kilicho karibu na ofisi ya Umoja wa Mataifa waliandamana kupinga hali inayoendelea nchini Sudan Kusini wakisihi Marekani iwasaidie.