Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakati wa ukweli kwa Syria umewadia- De Mistura

Wakati wa ukweli kwa Syria umewadia- De Mistura

Ingawa waasi wa Daesh nchini Syria wamesambaratishwa katika miji ya Raqqa na Deir-ez-Zour, bado ugaidi haujatokomezwa.

Hiyo ni kwa mujibu wa mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria, Staffan de Mistura akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hii leo kwa njia ya video kutoka Geneva, Uswisi, ambapo pia ametangaza kuanza kwa mazungumzo kuhusu Syria tarehe 28 mwezi ujao mjini Geneva.

Bwana De Mistura amesema kwamba sherehe za ushindi mji wa Raqqa umetuma ujumbe tofauti, ambapo licha ya kwamba maeneo mengi ya Syria kunashuhudiwa kupungua kwa ukatili, lakini kuzingirwa na mashambulizi ya anga yanaendelea.

Ameongeza kwamba ufikishwaji wa misaada ya kibinadamu na Umoja wa Mataifa na wadau kuwasilisha mahitaji ya kuokoa maisha bado ni changamoto akiongeza kuwa kuna haja ya kukomesha mapigano kote nchini.

(Sauti ya De Mistura)

“Ugaidi uko katika hatihati ya kushindwa lakini hautashindwa kwa njia za kisilaha pekee. Utaratibu wa kukabiliana na ukatili unakabiliwa na changamoto mara kwa mara lakini bado unafanikiwa. Baada ya Raqqa na baada ya Deir-ez-Zour nilikuwa nikisema, na labda utakumbuka, kutakuwa na wakati wa ukweli. Sasa ni wakati wa ukweli.”