Guterres ataja mambo muhimu CAR iweze kusonga mbele

26 Oktoba 2017

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameendelea na ziara yake huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR ikiwa leo ni siku ya tatu. Selina Jerobon na ripoti kamili.

(Taarifa ya Selina)

Nats…

Shamrashamra na mapokezi kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kila apitapo huko CAR.

Leo amekuwa na mazungumzo na Rais Faustin Archange Touadéra ambapo baadaye kwa pamoja walikutana na waandishi wa habari.

Rais Touadéra amesema nchi yake iko katika safari ndefu na ngumu ya ujenzi mpya, lakini wako katika mpango wa kitaifa wa kuleta mabadiliko.

Amesema mabadiliko hayo yanalenga kuleta wananchi pamoja na kujenga maisha yenye utu na kwamba wanaomba usaidizi kwa Umoja wa Mataifa.

Bwana Guterres kwa upande wake akapongeza vile ambavyo serikali imesimama kidete kuimarisha amani na usalama ili kazi ya ukarabati iweze kufanyika.

Amesema Umoja wa Mataifa utaendelea kutoa usaidizi ikiwemo kujenga uwezo wa ujumbe wake wa  kulinda amani, MINUSCA, kusaidia kuimarisha taasisi za kiserikali.

Na zaidi ya yote akatoa wito..

(Sauti ya Guterres)

“Kwanza ni kwa vikundi vilivyojihami, visalimishe silaha ili viweze kukubali kushiriki mchakato wa kisiasa nchini kwa kutambua kuwa ghasia kwa jamii haichagizi amani. Pili ni kwa viongozi wa kisiasa, kijamii na kidini wakubali kwa dhati maridhiano ya kitaifa. Nafahamu kuwa karibu mizozo yote ya kidini duniani inatokana na hila za kisiasa. Na tatu ni kwa jamii ya kimataifa, ni lazima kuwepo kwa rasilimali ili nchi iweze kuwa na mshikamano na wananchi waishi maisha yenye utu. Jamii ya kimataifa lazima itimize jukumu lake.”

Ziara ya Guterres huko Jamhuri ya Afrika ya Kati itamalizika Kesho ambapo atazungumza na waandishi wa habari kwenye mji mkuu Bangui.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter