Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mchakato wa makubaliano ya kimataifa ya uhamiaji wahamia Afrika

Mchakato wa makubaliano ya kimataifa ya uhamiaji wahamia Afrika

Mchakato wa mazungumzo baina ya serikali kuhusu makubaliano ya kuwezesha uhamiaji duniani kufanyika kwa kanuni stahili unaendelea leo huko Addis Ababa Ethiopia, ikielezwa makubaliano hayo ni fursa pekee ya kubadili fikra potofu kuhusu uhamiaji.

Akizungumza kwenye mkutano huo, mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa kuhusu uhamiaji wa kimataifa Louise Arbour amesema jambo muhimu la kuzingatia ni kwamba nchi nyingi zinahusika na uhamiaji.

Amesema nchi inaweza kuwa ni sehemu anayotoka mhamiaji, au kituo cha mpito cha mhamiaji au kituo cha mwisho ambako mhamiaji anahamia moja kwa moja.

Bi. Arbour amesema ni kwa mantiki hiyo kila nchi inapaswa kutambua kuwa inahusika kwa njia moja au nyingine kwa hiyo makubaliano ya pamoja yanaweza kuleta maslahi kwa pande zote tofauti na fikra za sasa ambapo kuna nchi zinazonufaika kuliko nyingine.

Ameweka bayana kuwa si kweli wahamiaji wengi wanakwenda nchi za magharibi akitolea mfano bara la Afrika ambako asilimia 52 ya wahamiaji wa nchi za Afrika wanahamia nchi nyingine za bara hilo na mara nyingi nchi jirani.

Kwa mantiki hiyo ametaka nchi za Afrika zitumie fursa ya makubaliano ya kimataifa ya uhamiaji kushughulikia masuala ya uhamiaji katika pande zote.

Mkutano huo umeandaliwa na kamisheni ya Umoja wa Mataifa kwa Afrika, ECA na utamalizika Kesho ambapo mashauriano ambayo yameanza mwezi Aprili mwaka huu yanatarajiwa kutamatishwa mwezi ujao.

image
Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu uhamiaji wa kimataifa Louise Arbour. Picha: UM/Eskinder Debebe