Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtandao mbovu wa usafiri majini wazidi kudumaza uchumi wa nchi maskini- UNCTAD

Mtandao mbovu wa usafiri majini wazidi kudumaza uchumi wa nchi maskini- UNCTAD

Mtandao dhaifu wa usafiri wa meli za biashara ni kikwazo kwa maendeleo ya nchi hususan zile maskini.

Hiyo ni kwa mujibu wa kamati ya biashara na maendeleo ya Umoja wa Mataifa, UNCTAD katika ripoti yake hii leo ya kutathimini usafirishaji majini kwa mwaka huu wa 2017.

Katibu Mkuu wa UNCTAD Dkt. Mukhisa Kituyi amesema kadri utandawazi unavyoshika kasi duniani, sekta za biashara, mawasiliano na fedha zinatagemea uwezo wa watu, kampuni na jamii kuweza kuwasiliana.

Hata hivyo anasema bado nchi maskini na zile ambazo hazina bandari zinakosa fursa ya kuunganishwa na mtandao wa usafiri wa meli za biashara na  hata zikiunganishwa bado gharama za usafirishaji bidhaa za biashara inakuwa ni kubwa.

Dkt. Kituyi amesema kinachohitajika sasa ni kuboresha bandari na mifumo ya kodi na ushuru ili kuweza kuvutia zaidi meli za kibiashara.

Halikadhalika kuweka takwimu kuhusu mitandao ya usafirishaji majini na kuijumuisha katika michakato ya kisera na hivyo kuwa sehemu ya majadiliano ya kibiashara na mipango ya kuendeleza na kuboresha miundombinu.