Guterres atoa wito kwa jamii ya kimataifa kusadia CAR
Akiendelea na ziara yake ya kikazi nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres leo amekutana na mwenyeji wake Faustin-Archange Touadéra kuzungumzia hatma ya nchi hiyo katika kuimarisha mshikamano na ushirikianao baina ya jamii ya kimataifa na nchi hiyo. Flora Nducha na taarifa kamili.
(TAARIFA YA FLORA)
Katika mazungumzo yao Guterres ameweka bayana nia ya Umoja wa mataifa na washirika wake ya kusaidia wananchi wa jamhuri ya afrika ya kati ili kujikwamua na hali ngumu ya kiuchumi wanayokabiliana nayo, usalama, na pia ujenzi mpya wa taifa hilo katika misingi ya amani akisisitiza
(António Guterres)
Ziara hii ni ziara ya mshikamano lakini ya ushirika na mshikamano, tuna ushirikiano wa kina na watu wa jamhuri ya Afrika ya Kati kwa sababu ya mateso , na matatizo mengi waliopitia. Lakini ujumbe muhimu wa ziara hii ni kwa jumuiya ya kimataifa, tunahitaji kujitolea kwa kwa kiasi kikubwa, sio tu kupunguza mateso haya, lakini kwa sababu kuna fursa ya kuijenga Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa amani, usalama na mafanikio kwa watu wake.
Aidha Bw Guterres amewaasa wana siasa na viongozi wa dini, wakae kwenye meza ya mazungumzo ya amani katika kutafuta muafaka wa migogoro ya kidini na kisiasa ya wenyewe kwa wenyewe.
Katibu mkuu alitoa wito kwa jamii ya kimataifa kupitia Baraza la Usalama kuongeza misaada itakayowezesha kuongeza nguvu kazi kwa MINUSCA katika ufanisi wa kazi yao ya kulinda amani wa wananchi.