Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano wa IAEA kutathimini mustakhbali wa uwezo wa nyuklia kufanyika Abu Dhabi

Mkutano wa IAEA kutathimini mustakhbali wa uwezo wa nyuklia kufanyika Abu Dhabi

Washiriki takribani 600 wakijumuisha mawaziri wa serikali, watunga sera na wataalamu kutoka kote ulimwenguni watakusanyika kwenye mkutano wa shirikala la kimataifa la nguvu za atomic IAEA huko  Emarati wiki ijayo ili kujadili mustakhbali wa uwezo wa nyuklia ikiwemo fursa na changamoto zake.

Mkutano huo wa kimataifa wa mawaziri kuhusu uwezo wa nyuklia katika karne ya 21 utakaoanza tarehe 30 Oktoba hadi tarehe Mosi Novemba Abu Dhabi, utatoa jukwaa la ngazi ya juu la mazungumzo kuhusu jukumu la uwezo wa nyuklia katika kukidhi mahitaji ya baadaye ya nishati, mchango wake katika maendeleo endelevu na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Washiriki kutoka nchi 60 wanachama wa IAEA na mashirika matano ya kimataifa pia watabadilishana mawazo katika masuala muhimu yahusuyo utengenezaji na usambazaji wa uwezo wa nyuklia.

Mkutano huo umeandaliwa kwa ushirikiano wa IAEA, shirika la nishati ya nyuklia (NEA) kwa ajili ya uchumi, ushirikiano na maendeleo na kwa hisani ya mwenyeji wa mkutano serikali ya Emarati kupitia wizara yake ya nishati na malaka ya udhibiti wa nyuklia.