Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM utaendelea kuenzi kazi ya walinda amani duniani- Guterres

UM utaendelea kuenzi kazi ya walinda amani duniani- Guterres

Akiwa Jamhuri ya Afrika ya Kati ambako amesherehekea na walinda amani wa Umoja wa Mataifa siku ya kuanzishwa kwa chombo hicho adhimu, Katibu Mkuu António  Guterres amesema hakuna jambo lenye maadili zaidi duniani kama kufanya kazi kulinda amani hata kama kitendo hicho kinamaanisha kupoteza uhai.

Amesema ni kwa muktadha huo anawapongeza walinda amani wa Umoja wa Mataifa ambao wamejitolea uhai wao kuhakikisha wanalinda amani hata katika maeneo ambako amani ina utata kama Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR.

Bwana Guterres amesema walinda amani wanapoteza maisha, wanajeruhiwa wakiwa wanasaka kulinda amani ya raia, raia ambao bendera ya Umoja wa Mataifa ndio kimbilio lao na ishara ya uhai kwao.

image
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akiwajulia hali baadhi ya walinda amani waliolazwa baada ya kujeruhiwa wakiwa kazini. (Picha:UN/Eskinder Debebe)
Kwa mantiki hiyo amesema anajivunia kuwa mmoja wa watumishi wa Umoja wa Mataifa sambamba na walinda amani hao akiwaeleza wao ni tegemeo la wengi ambao chombo hicho kinalenga kuwahudumia.

Katibu Mkuu amesema kujitoa kwao ni jambo ambalo litaenziwa kila wakati na Umoja wa Mataifa.

Akiwa kwenye mji mkuu wa CAR, Bangui,Katibu Mkuu aliweka shada la maua kukumbuka walinda amani waliopoteza maisha wakiwa kazini, alipata pia fursa ya kuzungumza na watendaji wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini  humo MINUSCA.