Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ofisi ya haki za binadamu yakemea uondoaji uwezo wa wasichana wenye ulemavu kupata watoto

Ofisi ya haki za binadamu yakemea uondoaji uwezo wa wasichana wenye ulemavu kupata watoto

Ofisi ya haki za binadamu wa Umoja wa mataifa imesema  vitendo vya kuwapatia dawa wasichana wenye ulemavu ili wasiweze kupata watoto ni ukiukwaji wa haki  za kibinadamu.

Catalina Devandas ambaye ni mtaalamu huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za watu wenye ulemavu amesema hayo leo katika ripoti yake kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.

Amesema jambo hilo si la kupuuzia na ofisi ya haki za binadamu haitafumbia macho vitendo vya kuwatoa mbegu za uzazi na kuwalazimisha kutoa mimba.

Aidha Bi. Devandas amependekeza kwamba serikali zote duniani zifutie mbali sheria zote zinazoruhusu utoaji wa kizazi kwa wasichana na wanawake vijana bila ridhaa yao na kuanzisha sheria za kulinda haki za wasichana wenye ulemavu.

Ameongeza kuwa  wasichana na vijana wenye ulemavu wana uwezo wa kujiendeleza wenyewe na kutambua uwezo wao mara tu wanapokua katika mazingira salama .