Siku ya Umoja wa Mataifa yaadhimishwa New York

Siku ya Umoja wa Mataifa yaadhimishwa New York

Umoja wa Mataifa hii leo umetimiza miaka 72 tangu kuanzishwa kwake ukijivunia usimamizi wa misingi yake mikuu minne iliyoridhiwa mwaka 1945 huko San Franscisco wakati chombo hicho kilianzishwa.

Katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani, maadhimisho yalitanguliwa na kusomwa kwa malengo ya chombo hicho kwa lugha sita rasmi, kiarabu, kichina, kirusi, kiingereza, kifaransa na kispanyola….

Malengo hayo ni kuendeleza amani na usalama duniani, kuimarisha ushirikiano katika kutatua masuala ya kiuchumi, kijamii, kitamaduni na kibinadamu, na kundeleza haki za binadamu bila kusahau ushirikiano wa baina ya nchi.

Maadhimisho yaliendana na tumbuizo kutoka bendi ya Umoja wa Mataifa na miongoni mwa washiriki ni Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Miroslav Lajčák na Naibu Katibu Mkuu Amina J. Mohammed .

image
Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Miroslav Lajčák (kushoto) na Naibu Katibu Mkuu Amina J. Mohammed (anayemfuatia) wakifuatilia maadhimisho ya siku ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani. (Picha:UN/)
Kwa upande wake Katibu Mkuu Antonio Guterres ameamua kuadhimisha siku ya leo na walinda amani wa Umoja wa Mataifa huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR na katika ujumbe wake amesema changamoto ni nyingi kama amani, usalama, njaa, vitisho vya nyuklia, lakini..

 (Sauti ya Guterres)

"Tuna nyenzo na rasilimali za kukabili changamoto hizi. tunachokihitaji ni utashi. Matatizo ya dunia yanavuka mipaka.Ni lazima tuzishinde tofauti zetu ili kubadili maisha yetu ya baadaye. Katika siku ya Umoja wa Mataifa, hebu, 'sisi binadamu', tuifanye ndoto hii itimie."