Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa waadhimisha kuanzishwa kwake hii leo

Umoja wa Mataifa waadhimisha kuanzishwa kwake hii leo

Leo ni siku ya Umoja wa Mataifa ambapo chombo hicho chenye wanachama 193 kinaadhimisha miaka 72 tangu kuanzishwa kwake baada ya vita Kuu ya pili ya dunia mwaka 1945.

Katika ujumbe wake kwa siku hii,  Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema maadhimisho yanafanyika wakati dunia inakabiliwa na changamoto nyingi kubwa.

Mathalani kuongezeka kwa migogro na kutokuwepo na usawa sanjari na hali mbaya ya hewa, ukosefu wa stahmala na vitisho vya  usalama ikiwemo silaha za nyuklia.

Hata hivyo amesema..

(Sauti ya Guterres)

“Tuna nyenzo na rasilimali za kukabili changamoto hizi. tunachokihitaji ni utashi. Matatizo ya dunia yanavuka mipaka.Ni lazima tuzishinde tofauti zetu ili kubadili maisha yetu ya baadaye. Katika siku ya Umoja wa Mataifa, hebu, ‘sisi binadamu’, tuifanye ndoto hii itimie.”

Katibu Mkuu wa Guterres ataadhimisha siku hii na walinda amani wa Umoja wa Mataifa huko Bangui, Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR ambapo katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa maadhimisho hayo yataongozwa na Naibu wake Amina J. Mohammed.

Hafla jijini New York, Marekani itaanza asubuhi kwa kusoma moja ya vipengele vya katiba ya Umoja wa Mataifa, ikifuatiwa na muziki na hatimaye kupandishwa kwa bendera ya Umoja huo.

Shughuli hiyo itashuhudia pia utoaji wa zawadi kwa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa ikiwa ni tuzo ya Katibu Mkuu ikiangazia vipengele vya ugunduzi na ubunifu, utendaji kazi wenye tija, usawa wa kijinsia na mabingwa wa utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

Hafla hiyo itaonyeshwa moja kwa moja kupitia televisheni ya mtandao ya Umoja wa Mataifa, http://webtv.un.org/