Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wananchi wa CAR wasema wanachotaka wao ni amani tu

Wananchi wa CAR wasema wanachotaka wao ni amani tu

Wakazi wa mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR wamesema wanachotaka wao hivi sasa ni amani ili waweze kuendelea na maisha yao ya kawaida baada ya miaka minne ya mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.

Wakazi hao wamesema hayo wakati wakizungumza na Idhaa ya Umoja wa Mataifa huko Bangui, mji mkuu wa CAR wakati huu ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António  Guterres anatarajia kuanza ziara Kesho Jumanne.

image
Katika kitongoji cha Bangassou, nchini CAR, maisha yanaendelea na shukrani kwa walinda amani wa Umoja wa Mataifa kupitia ujumbe wake, MINUSCA. (Picha:UN/Eskinder Debebe)
Miongoni mwa wakazi hao, Lawadi Ismael ambaye ni mwakilishi wa wakazi wa kitongoji cha PK5 kilichogubikwa na mapigano mwaka 2013 amesema hata wakati wa mapigano hakuondoka eneo hilo.

Amesema hivi sasa biashara inashamiri lakini mashambulizi dhidi ya waislamu ni lazima yakome kwani wanachotaka wao ni amani na maridhiano.

Bwana Ismael ameshutumu vikosi vya serikali kwa kutotilia maanani ulinzi wao huku akipongeza ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini humo MINUSCA kwa kuwapatia ulinzi.

Wakati wa mapigano moja ya daraja jijini Bangui ambalo lilijulikana kama daraja la kifo lililikuwa ndio mstari wa mapigano kati ya pande kinzani na sasa kuna amani na limepatiwa jina la daraja la Yakite likitumika kusafirisha abiria na mizigo bila hofu yoyote.

Kesho Katibu Mkuu Guterres pamoja na kutumia ziara yake kuadhimisha siku ya Umoja wa Mataifa, atatoa shukrani na kukumbuka walinda amani 12 waliouawa nchini  humo tangu mwezi Januari mwaka huu wakilinda raia.

Naye Mkuu wa kikosi cha MINUSCA Luteni Jenerali Balla Keita amesisitiza kuwa kamwe hakuna suluhu ya mzozo huo wa CAR kwa njia ya kijeshi bali kisiasa na kikosi chake kinasaidia kuweka mazingira bora ya ulinzi na usalama.