Tukizembea tutahitaji miaka 100 kutokomeza ndoa za utotoni- UNICEF

23 Oktoba 2017

Bila Ripoti mpya ya shirika la kuhudumia watoto ulimwenguni  UNICEF inasema bila hatua zaidi kuchukuliwa, dunia itahitaji miaka 100 zaidi ili kutokomeza ndoa za utotoni katika maeneo ya Afrika ya kati na magharibi.

Ripoti hiyo iitwayo Hatma ya ndoa za utotoni inasema licha ya kuongezeka maradufu kwa kiwango cha kutokomeza ndoa hizo, bado ukuaji mkubwa wa idadi ya watu na kuongezeka kwa vitendo hivyo kunatishia mafanikio na mamilioni ya watoto wako hatarani.

Fatoumata Ndiaye, ambaye ni Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF amesema ni lazima kutazama upya hatua zinazochukuliwa kwani hawawezi kuendelea kuona watoto wa kike wakikosa elimu, huduma ya afya na hata utoto wao.

Bi. Ndiaye amesema kadri mtoto wa kike anavyokuwa shuleni zaidi, ndipo uwezekano wa yeye kuolewa kabla ya kutimiza umri wa miaka 18 unapungua, halikadhalika kupata watoto akiwa bado mwenyewe ni mtoto.

Ripoti imetaja  nchi za Afrika magharibi na Kati zinazokabiliwa na ongezeko kubwa la ndoa za utotoni kuwa ni Niger, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad, Mali, Burkina Faso na Guinea.

Hata hivyo kuna nchi ambazo katika miaka 25 iliyopita zimefanikiwa kupunguza ndoa za utotoni kwa watoto wa kike nazo ni Gambia, Guinea Bissau, Togo, Ghana na Rwanda.

UNICEF imesema ndoa ya utotoni inatafsiriwa kama ndoa inayowahusisha watoto wenye umri wa chini ya miaka 18, na hivyo ni ukiukwaji haki za watoto na huwakosesha nafasi kumaliza shule, na pia  ni chanzo kikubwa cha maambukizi ya  Virusi Vya Ukimwi, VVU kwa watoto.