Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

AMISOM yaendesha mafunzo kukabiliana na utumikishwaji watoto vitani Somalia

AMISOM yaendesha mafunzo kukabiliana na utumikishwaji watoto vitani Somalia

Ujumbe wa Muungano wa Afrika nchini Somalia, AMISOM umefanya mafunzo kwa ajili ya kuzuia uandikishwaji wa watoto jeshini nchini Somalia

Mafunzo hayo ya siku 12 yalifanyika mjini Nairobi, Kenya yakiwaleta pamoja wahusika kutoka mamlaka ya kitaifa ya usalama nchini Somalia na maafisa wa serikali ya shirikisho.

Akizungumzia mafunzo hayo, mkuu wa masuala ya ulinzi, haki za binadamu na jinsia, AMISOM, Kareem Adebayo, amesema mafunzo ni muhimu kwa kila mtoto ambaye anazaliwa nchini Somalia kwani yuko katika hatari ya kuandikishwa jeshini na kutumikishwa vitani.

Aidha ametolea wito ulinzi wa watoto wote nchini Somalia kuwaepusha na kushirikishwa kwenye migogoro ya makundi yaliyojihami.

(Sauti ya Adebayo)

“Mafunzo ambayo tumekamilisha ni muhimu sana kwa sababu katika hali ya vita inayochukua sura tofauti, ambapo unakuta makundi ambayo yanaleta uzushi mara kwa mara mahali waliko; iwapo ni nchini Somalia waliko Al-Shabaab au Nigeria na Boko Haram, au Syria na ISIL, watu hawa wanawatumikisha watoto. Wanalisha sumu watoto ili waweze kufanikisha vitendo vyao vya kikatili.”

Bwana Adebayo ameonyesha matumaini akisema anatarajia washiriki wa mafunzo watapeleka stadi walizozipata nyumbani ili kusaidoa nchi katika kukabiliana na suala la watoto jeshi kwenye vita.