Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa na AU wafuatilia kwa karibu uchaguzi Kenya

Umoja wa Mataifa na AU wafuatilia kwa karibu uchaguzi Kenya

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Muungano wa Afrika, AU, Moussa Faki Mahamat, wanaendelea kufuatilia kwa ukaribu mchakato wa uchaguzi nchini Kenya zikiwa zimesalia siku chache kwa mujibu wa ratiba ya marudio ya uchaguzi huo tarehe 26 mwezi huu.

Taarifa ya msemaji wa Umoja wa Mataifa imeeleza kuwa kufuatia uamuzi wa  Mahakama Kuu ya Kenya wa Septemba mosi mwaka huu  kuhusu marudio ya uchaguzi wa urais nchini humo, Katibu mkuu Guterres na  mwenyekiti wa  AU kwa pamoja wameonyesha nia ya kusaidia Kenya kuhakikisha mchakato wa kuaminika na wa uwazi katika zoezi marudio hayo.

Aidha wamewaomba wadau ushirikiano  na Tume ya taifa ya uchaguzi ya na mipaka, IEBC, kama chombo chenye mamlaka ya kikatiba kutekeleza mchakato wa  uchaguzi .

Bwana Guterres na Bwana Mussa wanawahimiza viongozi  wa kisiasa wa vyama vyote  na wafuasi wao kulinda amani na kujiepusha na vitendo vya uvunjifu wa amani.

Pia wanasisitiza umuhimu vyombo vya  usalama kutotumia  nguvu  katika kutekeleza majukumu yao na kuheshimu uhuru wa wakenya  wote .